Taarifa iliyochapishwa katika gazeti rasmi la serikali ya Brazil imesema kuwa, Federico Meyer hataendelea kuwa balozi wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini huko Israel, bali ataiwakilisha Brasilia katika Kongamano la Geneva la Upokonyaji Silaha.
Sanjari na kukosoa hatua hiyo, Israel Katz, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel amesema kuwa Rais wa Brazil si mtu anayependwa na kwamba atasalia kuwa mtu asiyekaribishwa kuitembelea Israel mpaka abadilishe misimamo na kauli zake dhidi ya Israel.
Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil amekuwa akivifananisha vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na mauaji ya kimbari ya "Holocaust" yanayodaiwa kufanywa na Wanazi wa Ujerumani dhidi ya Mayahudi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.Kwa mujibu wa Da Silva, utawala huo unatekeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, na kwamba Umoja wa Mataifa na taasisi zake kama Baraza la Usalama lazima ziwe na ujasiri wa kuhakikisha kuwa inaundwa nchi huru ya Palestina.
Februari mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Brazil ilisema nchi hiyo imemrejesha nyumbani balozi wake wa Israel kwa ajili ya 'mashauriano' sanjari na kumuita balozi wa Tel Aviv mjini Brasilia, Daniel Zonshine kulalamikia kauli iliyotolewa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israel.
342/